MAMBO MATANO YA KUMFANYIA MPENZI WAKO ILI KUDUMISHA UHUSIANO















1. FANYA UCHAGUZI SAHIHI
Hapa ndipo watu wanapotakiwa kutumia akili zao mpaka zile za akiba, ukikosea hapa ni rahisi sana kuvurunda hapo baadaye. Uhusiano wenye nguvu, hujengwa na penzi la kweli. Acha kukurupuka, lazima ujihakikishie kwamba uliyenaye ni chaguo kutoka ndani yamoyowako.
Najua una maswali; kwamba utawezaje kumjua mwenye mapenzi ya kweli, hiyo ni mada ambayo nimeshaandika mara kadhaa katika ukurasa huu na gazeti damu na hili, Ijumaa. Kimsingi, kwa kufuata maelekezo hayo, mwenzi ambaye unatarajia kuwa naye katika maisha ya ndoa hapo baadaye, lazima msingi uwe ni uchaguzi sahihi.
Sikia, watu wengi waliokuwa na fedha, wamefilisika baada ya kuoa/kuoleawa na wenzi ambao si sahihi. Aidha, wapo wenye mafanikio makubwa sana, ambayo wameyapata baada ya kuoa/kuolewa na wenzi sahihi. Rafiki zangu, si jambo rahisi kumpata yule aliye sahihi. Inahitaji utulivu.
Yapo mengi sana ambayo unapaswa kuyaangalia, ambayo nimekwishaeleza sana katika makala zangu zilizopita. Wakati nahitimisha kipengele hiki, shika neno moja tu; unapomchagua mwenzi wa maisha yako, hakikisha ni yule aliye sahihi! Tuendelee na kipengele kingine.  

2. JIELEZE
Migogoro mingi baina ya walio kwenye uhusiano husababishwa na wenzi kutowafahamu vyema wenzao. Usiingie katika mkumbo huu, ni suala la kujieleza tu. Kumweleza mpenzi wako ulivyo, kutamfanya ajue vitu unavyopenda na usivyopenda. Aidha, kama unao udhaifu wowote wa kiafya na kadhalika, mweleze mwenzako.
Kumweleza kutamfanya ajiamini kuwa anapendwa. Kunaonesha unavyojiamini na unayetaka mwenzako ashirikiane na wewe katika hali uliyonayo. Si vibaya mwenzio kukufahamu kwamba una hasira sana. Yes! Maana akishajua hilo, ataacha utani unaokaribia kukuudhi maana anajua vizuri kuwa una hasira za karibu.
Ipo mifano mingi sana, lakini kikubwa cha kushika katika kipengele hiki ni kuwa mkweli kwa mwenzako kuhusu maisha yako. Acha kumdanganya kwamba familia yenu ina uwezo mkubwa, wakati ni wa kawaida. Kuwa mkweli, mapenzi si utajiri, ni hazina iliyojificha ndani ya moyo.
Kama anakupenda, anakupenda tu! Siku akigundua kwamba unamdanganya, pendo lake litapungua kwa kiasi kikubwa sana. Jieleze kwa uwazi na ukweli kutoka ndani ya moyo wako. Naye atakuheshimu na utakuwa umetengeneza mwanzo mzuri wa kuelekea kwenye ndoa isiyo na migogoro.
3. MPE UHURU

Wengi wanaamini kumbana mpenzi ni njia sahihi ya kumfanya awe mwaminifu, si kweli. Kuna wenye tabia ya kuvizia simu za wenzao na kuzipekua, si utaratibu mzuri. Mpe uhuru, usimbane! Kuonesha kumwamini sana mpenzi wako, kunamfanya naye aishi ndani ya uaminifu.
Kumchunga hakumnyimi kuendelea na mambo yake, sana sana atafanya kwa siri kubwa. Kumpa uhuru, kutamwogopesha, atajua yupo na mwaminifu ndiyo maana hafuatiliwi, hapo utakuwa umechochea naye awe mwaminifu kama wewe.  

4. ACHA PAPARA
Katika hatua za mwanzo kabisa za uhusiano wenu, hutakiwi kuwa na papara katika jambo lolote. Kila kitu kifanywe kwa utaratibu. Huna sababu ya kurukia mambo, hasa makubwa.
Wengi wamekuwa na haraka sana ya kukutana kimwili, haya ni makosa makubwa sana. Haraka ya nini kama unatarajia awe wako wa maisha. Ngoja nikuambie rafiki yangu, unapoanza kuulizia mapema mambo ya faragha, unamfanya mwenzako ashindwe kukuamini.
Kwanza, atahisi wewe upo kwa ajili ya kutaka kujistarehesha tu, lakini pia anaweza kufikiria kwamba unapenda sana mambo ya chumbani. Kumfanya agundue kasoro hiyo ni tatizo kubwa sana kwako.
Hata hapo baadaye mtakapoingia kwenye ndoa, ni rahisi zaidi kukumbuka mambo ya zamani, kwamba yupo na mtu anayependa sana mambo ya mahaba. Kwa maneno mengine, hata akihisi tu au kusikia kwamba una mtu mwingine pembeni, atapeleka moja kwa moja hisia zake kwenye kuamini moja kwa moja juu ya jambo hilo.
Papara si jambo jema kabisa kwa mwenzi ambaye unatarajia awe wako wa maisha. Tulia, mchunguze kwanza. Kumbuka unatakiwa kufikiria kuhusu mustakabali wa maisha yako ya baadaye, kama ndivyo, huna haja ya kuharakisha mambo ya mapenzi.
5. JENGA URAFIKI

Ukitaka kutengeneza uhusiano wenye nguvu, basi zingatia zaidi urafiki. Kumfanya mwezi wako rafiki ni silaha kubwa na yenye nguvu katika kuuimarisha uhusiano.
Mwenzi wako anapojiona kama rafiki, anakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumza chochote, ikiwemo matatizo na migongano mbalimbali kama rafiki zaidi.
Hawezi kukuficha siri zake. Atakuwa na wewe muda wote na atakusogeza karibu yake kwa kila kitu. Hata penzi lenu pia litakuwa na nguvu zaidi. Urafiki ni kila kitu ndugu zangu.
Acha tabia ya kumkaripia mpenzi wako, jenga mazoea ya kujadiliana zaidi kuliko kutumia kauli za ukali. Rafiki zangu, yote hayo niliyoyazungumza yanajengwa na jambo moja tu; urafiki!

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment